Serikali imesema kuwa Jiji la Dar es Salaam ndio litakalotumika katika mashindano ya AFCON mwakani kutokana na kuwa na miundombinu inayokidhi mahitaji ya michuano hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ambapo amesema kuwa baada ya wakaguzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afika (CAF) kuridhia kuwa jiji hilo lina miundombinu rafiki ikiwemo viwanja, hoteli pamoja na huduma za afya.

“Maandalizi ya AFCON 2019 yanaendelea vizuri tayari wakaguzi kutoka CAF wameshafanya ukaguzi wa awali na wamechagua Dar es Salaam ndio itakayotumika katika michuano hiyo ambapo mechi ya ufunguzi na ile ya fainali zitafanyika katika Uwanja wa Taifa”. amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha ameongeza kuwa viwanja vingine vitakavyomika ni uwanja wa Uhuru ambao upo katika ukarabati wa kuwekewa nyasi bandia na kurekebisha miundombinu mingine pamoja na uwanja wa Chamanzi ambao nao utafanyiwa ukarabati kulingana na matakwa ya CAF, na uwanja utakaotumika katika mazoezi mojawapo ni uwanja wa Jakaya Kikwete  Park.

Hata hivyo, Dkt Mwakyembe ameongeza kuwa maandalizi ya Kampeni ya Uzalendo na Utaifa yanaendelea ambapo mwaka huu kauli mbiu ni “Kiswahili Uhai wetu,Utashi Wetu” na  kilele kitakua Disemba 08 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

 

Mhadhiri UDOM anaswa 'akijaribu kupokea' rushwa ya ngono
Wananchi watakiwa kutokaa kimya