FC Barcelona inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Arsenal, Jorginho katika dirisha lijalo la majira ya baridi ambapo tayari imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake.
Kiungo huyu wa kimataifa wa ltalia anahusishwa kuondoka kwenye dirisha hli kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Washika Mitutu hao wa Jiji la London. Msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote.
Kwa mujibu wa tovuti ya ESPN, Jorginho mwenye umri wa miaka 31, anawindwa na FC Barcelona ambayo inataka kuziba mapengo ya Sergio Busquets na Franck Kessie walioondoka katika dirisha lililopita.
Barca ilimsajili Oriol Romeu kutoka Girona katika dirisha lililopita ili kuboresha eneo hilo, lakini mambo yanaonekana kwenda tofauti na Xavi anataka kiungo bora zaidi.
Mbali ya Jorginho, kwenye orodha hiyo pia kuna kiungo wa Bayern Munich, Joshua Kimmich, kiungo wa Liverpool, Thiago Alcantara na Guido Rodriguez kutoka Real Betis.
Mkataba wa Jorginho unatarajiwa kumalizika mwakani na kabla ya kutua Arsenal alikuwa akiwindwa na Juventus na baadhi ya timu nchini Italia.