Mambo mengi sana yamekuwa yanaongelewa juu ya wanaume wasaliti, kama, endapo mwanaume akakusaliti basi hakupendi, wengine wanasema mwanaume msaliti anakuwa amekosa heshima kwa mpenziwe na sio mwanaume mzuri.
Japokuwa mambo yote hayo yanayosemwa juu ya wanaume wasaliti yanaweza kuwa ya kweli, kunawanaume wengine sio wasaliti wa kudumu yani wana saliti mara moja moja.
Ni ukweli usio pingika kuwa kiwango cha usaliti kimeongezeka katika jamii yetu ikilinganishwa na miaka ya nyuma, na takwimu zinaeleza kuwa chanzo cha kuongezeka ni ukuaji wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano yaani matumizi ya simu.
“ Kamwe usijaribu kumpoteza mwanaume mwaminifu kwasababu ya kukusaliti mara moja au mbili tu” hii ni maada ambayo imekuwa ikijadiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu, lakini swali la kujiuliza je, usaliti wa mara moja moja unatakiwa kuvumiliwa kwenye mahusiano au ndoa?.
Moja kati ya hoja ambazo zimekuwa zikichangiwa ni kwa jinsi gani wanaume watachukua hatua endapo kibao kitageuka.
Kuna wengine wanaosema “ endapo mwanamke atamruhusu mpenzi wake kumsaliti mara moja moja, mwanamke huyo atakuwa hajikubali yeye mwenyewe, kwani mwanaume msaliti ni msaliti tu, hakuna anayesaliti kwa bahati mbaya, na hakuna usaliti wa mara moja moja , lazima utajirudia na kuwa tabia ambayo haiwezi kubadilika.
Robert Mkandawile ni mshauri wa masuala ya mahusiano, yeye anaamini kuwa usaliti unasababisha maumivu kwa wanawake na wanaume licha ya kuwa wanawake wamejijengea hali ya kusamehe mapema pindi wanapo salitiwa.
Lakini anasisitiza kuwa mapenzi ni kupendana kwa watu wawili bila kujali na bila kuwa na woga wa mmoja kumpoteza mwenzie, hivyo basi wanawake wanatakiwa kufahamu kuwa thamani yao haitegemei katika kumfanya mwanaume asimsaliti.
Na ameongeza kuwa kiuhalisia wanaume ni wabinafsi hivyo kwao sio rahisi kuvumilia usaliti unapotokea.
Kwa upande wake Mwanasaikolojia toka nchini Malawi, Daniel Chibwana ameeleza njia nzuri ya kukabiliana na usaliti katika mahusiano kwani usaliti ni dalili ya kuwepo kwa tatizo kwenye mahusiano au ndoa licha ya ukweli kuwa unasababu nyingi sana.
Yeye ameeleza kuwa hakuna mtu anaye saliti kwa bahati mbaya au bila kutarajia ( shetani kumpitia), usaliti hupangwa, hivyo basi sio sahihi kwa mtu kusamehewa kwa usaliti kwasababu hakujitambua anapofanya, nimuhimu kwa wapendanao kufanyia kazi chanzo au mzizi wa usaliti ulipo tokea.
Anasema wapenzi wanatakiwa kufuatilia na kuchambua nafasi zao kwa wenza wao ili kujua nini kinaweza kuwa chanzo cha usaliti na baada ya hapo wanatakiwa kuwa tayari kutatua au kukabiliana na chanzo hicho kwani wakishindwa kutatua watasababisha matatizo Zaidi.