Jiwe kubwa lenye uzito wa kilo 37 lililotumika kumpiga na kumuua mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu nchini Afrika Kusini baada ya kubakwa na genge la wahuni limewasilishwa mahakamani kama ushahidi.
Wakiwasilisha jiwe hilo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu iliyopo Cape Town, upande wa mashtaka ulieleza kuwa marehemu Hannah Cornelius (21) alipigwa na jiwe hilo kichwani baada ya vijana zaidi ya watatu kumbaka.
Aidha, waliiambia mahakama hiyo kuwa baada ya kumuua na jiwe hilo lililopasua fuvu la kichwa chake, kwa mujibu wa taarifa za kidaktari wabakaji hao pia walijaribu kumchinja ili kujiridhisha kama amekufa.
Watuhumiwa wa kesi hiyo wametajwa kuwa ni Vernon Witbooi, 33, Geraldo Parsons, 27, Nashville Julius, 29, na Eben Van Nieberk, 28, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji, ubakaji, utekaji na unyang’anyi.
Jiwe lililotumika kutekeleza mauaji hayo, lilibebwa na askari wawili wenye nguvu na kuwekwa kwenye meza kama kielelezo.
Hannah alibakwa na kisha kuuawa katika eneo la Stellenbosch nchini Afrika Kusini, baada ya vijana wanne kumvamia yeye pamoja na rafiki yake, Mei mwaka jana.