Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro – NCAA, imesaini mkataba wa Makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA- JKT), ya kuanza ujenzi wa Nyumba 5,000 za Wananchi wanaoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro, wanaoendelea kujiandikisha kuhama kwa hiari kwa kuzingatia misingi ya haki za Binadamu.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dkt. Freddy Manongi amesema mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2023 na tayari Serikali imeshatenga Shilingi 97 bilioni na kwamba unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi sita na hadi sasa jumla ya Kaya 1524 tayari zimeshajiandikisha kuhama kwa hiari.
Amesema, katika utekelezaji wa awamu inayofuata, pamoja na wananchi kuhamishiwa Nyumba zinazojengwa na Serikali pia Wananchi watapewa uhuru wa kuhamia mahali popote wanapotaka na Serikali itawapa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Tangu kuanza kwa zoezi hilo Juni, 2022, tayari makundi 19 yenye kaya zaidi ya 565 zenye watu 3097 wameshahama ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro sambamba na Mifugo yao zaidi ya 15,500 na Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi hilo, nyumba zaidi ya 500 zilijengwa.