Mara baada ya Droo ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa timu za wanawake kufanyika mjini Abdijan, Ivory Coast na JKT Queens kupangwa Kundi A na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, kiungo wa timu hiyo, Donisia Minja amesema hawahofii kupangwa kundi moja na timu hiyo.

Donisia akizungumza kwa niaba ya nyota wenzake wa JKT Quens amesema kwa sasa wanazingatia zaidi timu ya Twiga Stars itakayokuwa na mechi ya kufuzu Olimpiki kwa wanawake dhidi ya Botswana utakaochezwa Uwanja Wa Azam Complex Oktoba 26 lakini kundi hilo kwao sio tatizo.

JKT Queens ilipata nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ule wa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ikiifunga CBE ya Ethiopia kwa mikwaju ya Penati 5-4 baada ya dakika 90 kuisha zikiwa suluhu na sasa inajiandaa kwenda kushiriki fainali za Afrika ikiwa imepangwa kundi moja na Mamelodi, Athletico d Abidjan ya ivory Coast na SC Casablanca ya Morocco.

Kundi jingine la michuano hiyo itakayoanza kati ya Novemba 5-19 ni watetezi, AS FAR (Morocco), Ampem Darkoa(Ghana), Huracanes (Equatorial Guinea) na AS Mande ya Mali.

Alisema kama wachezaji kikubwa watasikiliza mbinu za Kocha wao Ester Chabruma akisaidiana na Bakar Shime nini anataka na kwamba kumaliza kundi hilo wakiwa nafasi ya pili sio kazi kwao kwani kila kitu kinawezekana.

“Kikubwa ni kumuomba mungu tuwe na afya njema na kuamka salama kwa sababu hakuna kinachoshindikana hatuhofii ukubwa wa Mamelodi kwa sababu mechi dakika 90.”

Amesema Donisia ambaye msimu uliopita wa ligi licha ya kuwa kiungo mkabaji lakini alimaliza nafasi ya pili kwa ufungaji akiwa na mabao 17 nyuma ya Jentrix Shikangwa (Simba) aliyefunga 19.

Wanajeshi wachukuliwa hatua kwa unyanyasaji wa kingono
Watanzania wanataka umeme - Dkt. Biteko