Baada ya kutwaa Ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Mkurugenzi wa Ufundi wa JKT Queens, Bakari Shime amesema watakwenda kufanya maandalizi kabambe ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuvuka rekodi iliyowekwa na Simba Queens msimu uliopita.
Akizungumza baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa CECAFA kwa kuibwaga CBE ya Ethiopia kwa mikwaju 5-3 ya Penati baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya fainali iliyochezwa Uwanja wa FUFA TC, Njeru nchini Uganda, Shime alisema baada ya kutwaa ubingwa huo wamepata tiketi sİ ya kuiwakilisha Tanzania tU kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, bali ukanda wote wa CECAFA, hivyo wanakwenda kufanya maandalizi kabambe ili waşiwaangushe watu wa Ukanda huo.
“Niwapongeze watanzania wote kwa ushindi huu, niwapongeze viongozi, benchi la ufundi na wachezaji, timu yetu ilikuwa inacheza mechi moja baada ya nyingine kulingana na ubora wa timu tuliyokuwa tunacheza nayo, katika mechi hii wameonyesha kiwango kikubwa sana hadi kufanikiwa kuwa mabingwa,” alisema Shime na kuongeza,
“Kwa sasa tumepata nafasi ya kuuwakilisha Ukanda wa CECAFA kwenye Ligi ya Mabingwa, tutarudi kukaa chini kuangalia pale ambapo tulitetereka tuparekebishe ili tukienda tuvuke pale ambapo timu ya Tanzania ilifika msimu uliopita,” alisema Shime.
Naye kocha wa timu hiyo, Ester Chabruma amesema haikuwa kazi rahisi kutwaa ubingwa wa CECAFA mbele ya CBE ambayo ameitaja kuwa ni moja kati ya timu bora kwenye ukanda huu.
“Tunashukuru kwa kuchukua Ubingwa, mechi yetu ilikuwa nzuri na yenye Ushindani, nilisema tangu awali CBE ya Ethiopia ni timu nzuri na kutakuwa na upinzani na kweli imekuwa hivyo, lakini sisi tulikuwa bora zaidi,” amesema Chabruma.
Hii ni mara ya pili kwa timu ya Tanzania kutwaa ubingwa wa CECAFA ambapo msimu uliopita, Simba Queens ilitwaa Ubingwa huo kwa kuifunga She Corporate ya Uganda bao 1-0 na kwenda kuuwakilisha Ukanda wa CECAFA kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa nchini Morocco ambako ilimaliza kwenye natasi ya nne.