Klabu ya Soka ya JKT Queens imetangaza kujiweka sawa na kufanya vyema katika mchezo wa Nusu Fainali ya michuano ya CECAFA na kufuzu Fainali kisha kutwaa taji.
Hayo yamesemwa jana na Afisa Habari wa JKT Queens, Masau Bwire alipozungumza kuhusu maandalizi ya kikosi chake kinachojiandaa na mchezo wa Nusu Fainali.
JKT Queens itajitupa imbani kesho Jumatano (Agosti 23) katika mechi dhidi ya mshindi wa pili wa kundi A ambaye anaweza kuwa Buja Queens au Kampala Queens, katika michuano wanawake iliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), inayoendelea jijini Kampala, Uganda.
Bwire amesema pamoja na kusubiri timu ya kucheza nayo nusu fainali, JKT Queens imejipanga yema kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania na kuwania taji.
Amesema timu ipo katika hali nzuri na wachezaji wanaendelea kufanya mazoezi makali na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo unaofuata na kujiweka katika nafasi ya kukata tiketi ya kucheza fainali.
JKT Queens ilianza mashindano kwa kuichapa As Kigali ya Rwanda mabao 2-1 kisha kuifunga bao 1-0 New Generation ya Zanzibar kabla ya kuichezesha gwaride Vihiga Queens kwa bao 1-0.
Timu hiyo ya maafande, imevuna alama tisa katika Kundi B baada ya kushinda michezo yote dhidi ya Vihiga Queens ya Kenya, New Generation ya Zanzibar na AS Kigali ya Rwanda huku ikikubali kufungwa bao moja.
Iwapo JKT Queens itashinda mchezo wa Nusu Fainali, itakata tiketi ya kucheza Fainali na ikitwaa kombe itakwenda kushiriki Fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.