Baada ya klabu tatu za mkoa wa Dar es salaam kujihakikishai nafasi ya kupanda daraja zikitokea ligi daraja la kwanza hadi ligi kuu kwa msimu wa 2018/19, chama cha soka mkoani humo DRFA kimezipongeza klabu hizo.
Dar es salaam imeongeza klabu nyingine tatu katika ligi kuu ambazo ni JKT Tanzania, KMC na African Lyon na zinaungana na klabu nyingine tatu za mikoa mingine.
Klabu nyingine tatu zilizofanikiwa kupanda daraja ni Alliance Sports Club ya mwanza, Biashara FC ya mkoani Mara na Costal Union ya Tanga.
DRFA imezipongeza klabu za mkoa wa Dar es salaam kwa kuziandikia ujumbe maalum ambao umesambazwa katika vyombo vya habari.
Ujumbe wa DRFA kwa klabu za JKT Tanzania, KMC na African Lyon.
Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kinazipongeza timu za JKT Tanzania, KMC na African Lyon kwa kufanikiwa kuwa miongoni mwa timu sita zilizopanda ligi kuu daraja (VODACOM Premier League) kwa msimu wa 2018/19.
DRFA inaamini mafanikio waliyopata timu za JKT, KMC na African Lyon yametokana na uongozi bora pamoja na mipango mizuri waliyojiwekea katika vilabu vyao. Kwahakika wameutendea HAKI Mkoa wa Dar es Salaam.
Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kinawahakikishia vilabu hivyo vilivyopanda na vilabu vingine vilivyopo katika ligi kuu (VODACOM Premier League) kuwa DRFA itaendeleza ushirikiano uliopo na uongozi wake pamoja na kamati nzima ya utendaji ya vilabu hivyo katika masuala mbalimbali ya kuendeleza soka la Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla.
Kwa niaba ya kamati ya utendaji ya DRFA na familia ya mpira wa Miguu katika mkoa wa Dar es Salaam tunawapa pongezi za dhati kwa mafanikio hayo mliyoyapata na kuomba kuitumia nafasi hiyo kuweza kujipanga na kuwa na maandalizi mazuri kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi katika ligi kuu (VODACOM Premier League) msimu wa 2018/19 na inayofuata.
Mbali na pongezi hizo kwa vilabu vya Dar es Salaam vilivyopanda ligi kuu (VODACOM Premier League), DRFA pia imeipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Walace Karia pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa usimamizi mzuri wa Ligi ya daraja la kwanza (FDL) msimu wa 2017/18 iliyomalizika jana bila ya viashiria vyovyote vya upangaji wa matokeo.
Nawasilisha.
Almasi J. Kasongo,
Mwenyekiti
Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa Wa Dar es Salaam (DRFA)