Uongozi wa JKT Tanzania rasmi umethibisha kikosi chao kitautumia Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga kama uwanja wao wa nyumbani katika michezo yote ya Ligu Kuu Tanzania Bara hadi pale uwanja wao wa Meja Jenerali Isamuyo uliopo Mbweni Dar es salaam utakapokamilika baada ya matengenezo makubwa yanayoendelea kufanywa.
Hayo yameelezwa na Afisa Habari na Mawasiliano wa JKT Tanzania, Masau Bwire katika Mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika leo Jumatano (Septemba 27) Mjini Shinyanga.
Masau amesema wameamua kuuchagua uwanja wa CCM Kambarage kama uwanja wao wa nyumbani kwani wanataka maeneo yote nchini yanapata fursa ya kushuhudia Soka, hivyo furaha ya JKT Tanzania ni kuona wakazi wa Shinyanga wanapata furaha ya Soka hivyo amewaomba wakazi wa Mkoa huo kuipa ushirikiano timu yao.
“Tutatumia uwanja huu hadi uwanja wetu utakapokamilika matengenezo, Uwanja wa CCM Kambarage umepitishwa na TFF kwa ajili ya kutumika kwa ajili ya mechi za ligi kuu ya NBC. Na tutaanza kuutumia uwanja huu katika Mchezo wetu na Kagera Sugar utakaofanyika keshokutwa Ijumaa (Septemba 29), ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme.”
“Tunaomba wakazi wa Shinyanga waichukue na kuipokea JKT Tanzania kama timu ya nyumbani na kuipa ushirikianao wote katika kuendelea kutumia uwanja wa CCM Kambarage.” amesema Bwire.
“Double K ni kichapo cha kizalendo kiheshimike kwa kuwa kila timu itakayofika hapa lazima ipate kichapo. Mechi ya Ijumaa na Kagera Sugar ni kichapo cha kizalendo, Kagera Sugar tutaipa Double K kwani tuna kikosi bora na makini na wachezaji wenye vipawa zaidi.” amesema
“Tumepanga kiingilio ni Tshs 2000/= kwa mzunguko na Jukwaa kuu ni Tshs 3000/= kwa maana ya jukwaa kuu. Pia Mfumo wa N Card utatumika ili kusaidia kutoa huduma kwa mashibiki kukata tiketi zao.”
“Tunatumia N Card ili kuepusha msongamano na malalamiko na tumewasiliana na mamlaka husika wa kutekeleza jukumu hilo kutoka Dar es salaam na ofisi ya TTCL na utaratibu wa kuuza tiketi utafanyika katika vituo vya Soko Kuu, Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga na ofisi za TTCL Shinyanga na siku ya mechi mageti katika uwanja wa CCM Kambarage yatafunguliwa kuanzia saa 4:00 asubuhi.
“Tungependa mashabiki wetu waje na sura ya JKT siku ya mechi kwa kuvaa jezi zenye ubora ambazo zinapatikana kwa Tshs 35,000/= na kofia kwa Tshs 10,000/=” ameeleza