Klabu ya JKT Tanzania imetangaza rasmi kuwa itautumia Uwanja wa Kambarage Shinyanga kama dimba lake la nyumbani katika mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara, pindi utakapofunguliwa na Bodi ya Ligi nchini, TPLB.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Kapteni Speratus Ngemeke Lubinga, amesema  kuwa wameamua hivyo baada ya kupokea ombi kutoka Serikali ya mkoa huo pamoja na mashabiki wa soka mkoani Shinyanga.

Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kutoka Championship, ilikuwa inautumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam, kwenye mechi zake mpaka ilipofanikiwa kupanda Ligi Kuu.

“Tuliitikia wito kutoka Serikali ya Mkoa wa Shinyanga, lakini pia tuliitikia wito wa Bodi ya Ligi, baada ya kupita kuukagua uwanja walituambia tuwe karibu na wamiliki wa uwanja ambao kwa sasa wanautengeneza kwa ajili ya matumizi ya Ligi Kuu, na baada ya maelekezo hayo tuliwasiliana na mkoa, wakatuambia twende tukaone hayo marekebisho ambayo Bodi ya Ligi wanataka yafanyike,” amesema katibu huyo.

Amesema iwapo utafunguliwa, watacheza mechi zao zote za nyumbani msimu huu mkoani humo.

Timu hiyo tayari imecheza mechi moja tu ikiwa ugenini Jumanne iliyopita, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo FC na kupata ushindi wa bao 1-0.

Mmoja wa wanaosimamia uwanja huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema TPLB iliwashauri kuondoa vipara viwili uwanjani hapo ambavyo vilikuwa maeneo ya kupigia kona na tayari wameshapanda nyasi, sehemu ya benchi ya kukaa makocha na wachezaji wa akiba na kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji.

Habari kutoka Shinyanga zinasema tayari wakaguzi wameshafanya kazi yao na kujiridhisha, hivyo wakati wowote unaweza kuruhusiwa kutumika kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu.

KMKM matumaini kibao Michuano ya Afrika
Kanuni ya muda yamkera Mikel Arteta