Kikosi cha JKT Tanzania kitaanza rasmi kuutumia Uwanja wa CCM Kambarage ulioko Shinyanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa Septemba 29, mwaka huu, imefahamika.
Mechi hiyo itakuwa ni ya kwanza ya nyumbani kwa JKT Tanzania na inatokana na kukamilika kwa maboresho kama walivyoshauriwa na Bodi ya Ligi.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Kapteni Godwin Ekingo, amesema kikosi chao kilitarajiwa kufika Shinyana jana usiku kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi hiyo ya raundi ya tatu.
“Timu imeshatoka Dar itawasili Shinyanga muda wowote, tuliomba hapa kuwa ndiyo Uwanja wetu wa nyumbani,” alisema Ekingo ambaye timu yake ina pointi tatu ilizopata ugenini katika mechi ya kwanza dhidi ya Namungo.
Naye Meneja wa Uwanja wa CCM Kambarage, Lawrence Manotta, alisema Uwanja huo kwa sasa upo tayari kutumika baada ya kukamilisha maboresho ambayo walitakiwa kuyafanya.