Mabingwa wa Soka nchini Hispania FC Barcelona wana uhakika wa kukamilisha usajili wa beki wa pembeni kutoka nchini Ureno Joao Cancelo.
Mchezaji huyo mwenye Umri wa miaka 29, hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mabingwa wa Soka nchini England ‘Man City’ chini ya Kocha Pep Guardiola.
Alitumia kipindi cha pili cha msimu uliopita kwa mkopo akiwa FC Bayern Munich, ambao walikataa kumsajili kwa uhamisho wa kudumu.
Baada ya mazungumzo mazuri mwishoni mwa juma, Earca sasa wanakaribia kufikia makubaliano ya kumsajili Cancelo kwa mkopo kwa msimu huu.
Vyanzo vya habari vimethibitisha kwamba FC Barcelona itagharamia sehemu kubwa ya mshahara wa Cancelo katika msimu huu na pia wamekubali chaguo lenye thamani ya Pauni Milioni 30 ili kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu msimu ujao.
Cancelo alipata ofa kutoka Saudi Arabia na pia kulikuwa na nia kutoka Ulaya, ikiwa ni pamoja na Arsenal, lakini ofa ya kucheza katika kikosi cha kwanza chini ya Xavi huko Barca lilikuwa chaguo la kwanza la mchezaji huyo.
Nyota huyo huenda akapata nafasi ya kuungana na mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Ureno, Joao Felix, huku mazungumzo yakiendelea kuhusu mkataba wa mkopo na Atletico Madrid.
Makamu wa Rais wa FC Barcelona, Rafa Yuste, hivi karibuni alikiri kwa Movistar kuwa klabu hiyo ilikuwa na matumaini ya kuwapata Cancelo na Felix.
“Ni jambo la kujivunia kwa klabu kwamba Joao Felix anazungumza kwa njia hiyo kuhusu FC Barcelona, lakini kuna operesheni mbili ambazo Xavi na Deco wanapaswa kushughulikia,” alisema Yuste.