Mashabiki wa Atletico Madrid, wamefuta jina la Joao Felix kwenye bango lao baada ya kuonyesha wazi kwamba ana nia ya kujiunga na FC Barcelona.

Mashabiki hao walichukizwa kwa sababu FC Barcelona ni wapinzani na wasingekubali kuona nyota huyo akijiunga na miamba hiyo ya Catalunha.

Felix aliwakera mashabiki baada kuweka wazi kwamba anatamani ajiunge na FC Barcelona huku akisema: “Barcelona ndio klabu ya kwanza kuichagua, ningependa kuichezea siku za usoni. Kama ikitokea itakuwa ndoto kubwa katika maisha yangu ya soka.”

Lakini cha kushangaza kauli hiyo iliwachukiza mashabiki wa Atletico na wakapigia mstari jina la Felix kwenye bango ambalo lipo nje ya uwanja wao.

Felix mwenye umri wa miaka 23, amerejea Madrid baada ya kucheza kwa mkopo Chelsea msimu uliopita lakini hatma yake bado haileweki mpaka sasa.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alirejea baada ya kutemwa na kocha mpya wa Chelsea, Mauricio Pochettino akidai kwamba hana mipango naye msimu ujao.

Msimu uliopita alifunga mabao manne katika mechi 20 huku pia akilimwa kadi nyekundu katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Awali alikuwa na matarajio ya kusajiliwa jumla na Chelsea lakini Pochettino akampiga chini.

Mlinda Lango wa Real Madrid, Thibaut Courtois aliwahi kufanyiwa vitendo hivyo alipoondoka Chelsea na kutua Santiago Bernabeu.

Wahalifu 106 watupwa Gerezani Arusha
Kenya, Dubai kusaini uwekezaji - Zambia, DRC zanyatia fursa UAE