Mshambuliaji Joao Felix amesema hakuwahi kuzoea maisha ya Atletico Madrid au mipango ya Kocha, Diego Simeone baada ya kuanza yema soka lake na FC Barcelona.
Félix mwenye umri wa miaka 23, amefunga mara tatu katika mechi zake mbili za kwanza alizoanza Barca baada ya kujiunga na klabu hiyo kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Atletico mapema mwezi huu.
Mshambuliaji huyo wa Ureno alisasajiliwa Atletico akitokea Benfica kwa euro milioni 126 mwaka 2019, lakini hakuwahi kufikia matarajio katika misimu minne aliyocheza chini ya Simeone.
“Mambo yanapoenda vibaya katika soka kwa mtu, lazima ufanye mabadiliko,” alisema Félix katika mahojiano na Mundo Deportivo.
“Nilifanya hivyo kabla ya kwenda Chelsea (kwa mkopo katika kipindi cha pili msimu uliopita) na sasa kuja FC Barcelona kwa sababu sikuwa naendelea vizuri kule Atletico.
“Sikukubaliana na mawazo ya klabu au kocha, lakini kila mara nilijaribu kufanya kitu bora niwezavyo. Nimekuwa na nyakati nzuri huko pia.”
Félix alikataa kwenda Saudi Arabia akisubiri nia ya Barca, na hatimaye makubaliano yalifikiwa siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho wa majira ya joto.
Ili kukamilisha usajili huo wa mkopo huo, ilibidi Felix akubali kukatwa kiasi kikubwa cha mshahara wake iliyotokana na matatizo ya kifedha ya Barca.
“Ni kweli niliacha sehemu kubwa ya mshahara wangu, lakini nilihitaji mabadiliko,” aliongeza.
“Nilihitaji kufika mahali ambapo naweza kucheza mtindo wangu wa soka na nimekuwa nikisema kila mara nadhani hapa ni mahali pazuri.
“Mambo yanakwenda vizuri, sikutarajia kuanza vizuri, na ilikuwaa ni juhudi nilizohitaji kufanya ili kupata furaha ya kucheza soka tena.”
Félix alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Real Betis wikendi iliyopita na kufuatiwa na mabao mawili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Royal Antwerp kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita.
Matokeo hayo yalimsukuma Kocha wa Barca, Xavi Hernandez kudai timu yake inacheza soka lao bora tangu achukue mikoba yake mwaka 2021.
Kusajiliwa kwa Félix kumechangia kuimarika kwa kiwango hicho, lakini mchezaji mwingine mpya aliyesajiliwa, João Cancelo, pia amekuwa na jukumu muhimu tangu ajiunge naye kwa mkopo akitokea Manchester City.
“Kwa upande wa ubora, nadhani ndiye belki bora zaidi wa pembeni ambaye nimewahi kucheza naye,” alisema Félix kuhusu klabu na mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Ureno, Cancelo.