Mlinda mlango kutoka Uingereza Joe Hart, amesema hajutii kujiunga na klabu ya Torino ya nchini Italia kwa mkopo wa muda mrefu akitokea Manchester City.

Hart amesema huenda mashabiki wengi wa soka duniani wanaamini anajutia kusukumwa kufanya maamuzi hayo kufuatia utaratibu wa meneja mpya wa Man City Pep Guardiola, lakini jambo hilo kwake analichukua poa.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 29, alilazimika kupelekwa Torino kwa mkopo mwishoni mwa mwezi Agosti, kufuatia kiwango chake kutomridhisha Guardiola ambaye aliamua kumsajili mlinda mlango kutoka nchini Chile Claudio Bravo akitokea FC Barcelona.

“Soka ni mchezo usiofungamana na mazingira yanayokuzunguuka, unaweza kucheza popote pale na bado kiwango chako kikaonekana, hivyo siwezi kujutia kuondoka Man City kwa mkopo wa muda mrefu,” Hart alivieleza vyombo vya habari vya Uingereza.

“Kwa bahati mbaya zaidi sikujali ninapokwenda ni mahala gani, nilitambua ninajukumu la kucheza soka kwa kiwango cha hali ya juu na sasa nipo safi, na nina uhuru wa kushirikiana na wachezaji wengine wa Torino tunapokua uwanjani.

“Nimebaini Torino ni mahala sahihi kwa mchezaji kama mimi. Ninazungumza haya sidanganyi hata kidogo kwa sababu mimi ndiye muhusika na mazingira yanayonizunguuka huko Italia. Torino ni mahala pazuri kweli kweli, na katu sitokua mchoyo wa shukurani kwa mashabiki ambao kila leo wamekua wakikubaliana na uwezo wangu pamoja na timu yao kwa ujumla. Aliongeza Hart

Hart alilazimika kurejea nyumbani kwao Uingereza, baada ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, ambacho tangu mwishoni mwa juma lililopita kimekua kikikabiliwa na michezo ya kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

DRC Yamponza Javier Clemente, LFF Yamfungashia Virago
Video: Baraka The Prince akerwa na utani wa Stan Bakora, "iwe mwanzo na mwisho"