Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC John Bocco amesema kuwa wachezaji wote wamekubaliana kufanya vizuri kwenye michezo ya Ligi Kuu iliyosalia ili kutimiza malengo ya timu baada ya kupata somo kimataifa.
Timu hiyo imebaki kwenye mashindano mawili ambayo ni Kombe la Tanzania Bara ‘ASFC’ ikiwa hatua ya Nusu Fainali na Ligi Kuu ambapo ipo nafasi ya pili, ikitanguliwa na Young Africans.
Katika Michuano ya Kimataifa Simba SC imetotea hatua ya Robo Fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kuondolewa na mabingwa watetezi Wydad AC, Ijumaa (Aprili 28) kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Bocco mwenye mabao 9 na pasi moja ndani ya Ligi Kuu akiwa ni kinara kwa mastaa wenye hat-trick nyingi Bongo ambazo ni mbili kwa msimu wa 2022/23 amesema kuwa mpango mkubwa ni kufanya vizuri kwenye michezo yao.
“Tumepata somo kubwa kwenye mashindano makubwa na wachezaji tumekubaliana kuwa mechi zilizobaki kupambana kupata matokeo hasa kwenye ligi pamoja na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
“Kikubwa ni kupata ushindi kwani tunaamini tutafanyia kazi yale mazuri na mabaya nayo tuna kazi ya kuboresha ili tuwe imara wakati ujao,” amesema Bocco