Baada ya kuiwezesha timu ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Njombe Mji FC katika uwanja wa Sabasaba mjini Njombe hapo jana, nahodha na mshambuliaji wa Wekundu hao wa Msimbazi, John Bocco amesisitiza mshikamano kwa viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki, ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Tanzania bara.
Bocco alifunga mabao mawili ya ushindi katika mchezo huo na kuifanya Simba kujikita kileleni mwa msimamo wa ligikuu ya soka Tanzania bara kwa kufikisha alama 49 ikiwa juu kwa pointi tatu dhidi ya Young Africans wenye alama 46.
Mshambuliji huyo amesema licha ya ushindi wa jana, bado ushindani katika ligi ni mgumu, hivyo hakuna njia ya mkato zaidi ya kuendelezwa kwa mshikamano uliopo ndani ya klabu yao.
Hata hivyo msambuliji huyo aliejiunga na Simba akitokea Azam FC mwishoni mwa msimu uliopita, amesema suala la ubingwa bado ni gumu kwa kila timu zinazotajwa, na kwa hatua hiyo hawawezi kubweteka.
“Nichukue nafasi hii kuwataka Wanasimba wote kuendelea kushikamana katika kipindi hiki mpaka mwisho wa msimu ili tupate ubingwa,” alisema Bocco.
Simba italazimika kutwaa ubingwa wa Tanzania bara, ili kujihakikishai nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, baada ya kuondolewa mapema katika michuano ya kombe la shirikisho (Azam Sports Federation Cup).