Aliyekua nahodha wa timu ya taifa ya England na klabu ya Chelsea John Terry ametangaza rasmi kustaafu soka huku akiacha kumbukumbu kubwa katika tasnia ya soka lake.
Terry anaondoka katika medani ya soka, baada ya kuwa beki na nahodha aliyedumu kwa muda mrefu katika kikosi cha Chelsea, ambacho alikitumikia katika michezo 717 na kushinda mataji matano ya ligi kuu ya England.
Ametangaza kuachana na soka, akiwa na klabu ya Aston Villa inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini England, ambayo ilimsajili misimu miwili iliyopita akitokea Chelsea.
Hata hivyo taarifa zinasema kuwa, beki huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 37, huenda akasalia Villa Park na kuteuliwa kuwa meneja msaidizi, kufuatia tetesi za aliyekua nahodha na mashambuliaji wa Arsenal Thierry Henry kufikiriwa kupewa jukumu la benchi la ufundi.
Baada ya kutangaza maamuzi ya kustaafu soka, Terry alitumia ukurasa wake wa Instagram kuandika ujumbe kwa ndugu, jamaa, marafiki na mashabiki wake: “Baada ya miaka 23 ya kucheza soka la ushindani, leo nitatangaza rasmi kuachana na mchezo huu kama mchezaji, Nimefanya maamuzi haya kwa muda muafaka. Sina budi kutoa shukurani kwa kila mmoja aliyeniwezesha kucheza soka kwa umakini kwa muda wote.
“Mke wangu Toni na watoto wangu wawili Georgie na Summer, kwa kuwa muhimili mkubwa kwenye mafanikio niliyoyapata – Ninaamini nisingeweza kufanya yote niliyoyafanya kama sio nyinyi kunipa moyo, na kunipongeza pale nilipofanya vyema.”
“Ninawashukuru wazazi wangu, Sue na Ted kwa kunipa malezi bora na kuniendeleza katika mchezo wa soka pale nilipoonyesha kipaji tangu nikiwa kijana mdogo sana, mliniwezesha kufanikisha lengo langu.”
“Kaka yangu Paul, ninakushukuru kwa msaada na ushauri wako katika kipindi chote cha uchezaji wangu – pia niseme ahasante kwa familia yangu yote na marafiki popote pale walipo kwa ushirikiano wenu.”
“Nikiwa na miaka 14, nilifanya maamuzi magumu ya kusaini kwenye klabu bora ya Chelsea. Tendo hili litaendelea kuwa kumbukumbu katika maisha yangu yote, limeniwezesha kufanya nilichokikusudia, leo mashabiki wanatambua mchango wangu katika soka la England, kwa sababu ya klabu hii.”
“Hata nilipojiunga na Aston Villa, nilitambua maamuzi yangu yalikua sahihi sana, nilitamani kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wangeweza kuisaidia klabu hii kurejea ligi kuu, tulijaribu msimu uliopita, lakini hatukufanikiwa, ninaahidi kuwa bega kwa bega na kila mmoja anaehusika na klabu hii, ili kufanikisha lengo hili.”
John Terry na Thiery Henry
Aston Villa ilifanikiwa kufika fainali katika hatua ya mtoano ya ligi daraja la kwanza, lakini kwa bahati mbaya ilifungwa bao moja kwa sifuri na Fulham, na kushindwa kufanikisha lengo la kupanda daraja na kucheza ligi kuu msimu huu wa 2018/19.
Kwa upande wa timu ya taifa Terry amefanikiwa kucheza michezo 78. Mafanikio aliyoyapata wakati wote ni kutwaa ubingwa wa ligi ya England mara tano akiwa na Chelsea, ubingwa wa kombe la chama cha soka (FA CUP) mara tano, Kombe la Ligi (Carabao Cup) mara tatu. Pia alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ulaya (Champions League) na Europa League mara moja.