Beki na nahodha wa klabu ya Chelsea John Terry, atakosa mchezo wa mwishoni mwa juma hili ambapo The Blues watakuwa na kibarua cha kuwakabili majogoo wa jiji kwenye uwanja wa Stamford bridge siku ya ijumaa.

Terry alimaliza mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Swansea City akiwa anachechemea, baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

Baada ya mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili, meneja wa Chelsea Antonio Conte alionyesha kuwa na wasi wasi na afya ya Terry, lakini aliwaambia waandishi wa habari kuwa na subra hadi majibu ya vipimo yatakapotolewa.

“Siwezi kufahamu ameumia kwa kiasi gani, lakini nina uhakika kesho (jumatatu) tutajua kwa kina, baada ya kufanyiwa vipimo,” Alisema Conte.

Hata hivyo jana klabu ya Chelsea ilitoa taarifa za maendeleo ya Terry ambazo zilieleza wazi kwamba, beki huyo ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya England hatoweza kuwa sehemu ya kikosi cha The Blues katika mchezo ujao.

Taarifa hizo ziliongeza kuwa, beki huyo mwenye umri wa miaka 35, atakua nje kwa muda wa siku 10 na ana matumaini makubwa ya kucheza mchezo wa ligi wa Septemba 24, ambapo kikosi cha Chelsea kitakabiliana na Arsenal.

Kutokuwepo kwa Terry katika mchezo wa siku ya ijumaa dhidi ya Liverpool, kutatoa nafasi kwa David Luiz aliyerejeshwa klabuni hapo akitokea Paris Saint-Germain kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 32 kucheza sambamba na Garry Cahil.

Video: Waziri Mkuu apokea zaidi ya sh. bil. 1.4 kwaajili ya maafa tetemeko la Kagera
David Ospina Amkuna Arsene Wenger