Beki Joleon Lescott ameungana tena na David Moyes baada ya kukubali kusajiliwa kwa mkataba wa muda mfupi na klabu ya Sunderland.
Wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Everton, lakini Lescott aliondoka na kujiunga na klabu ya Man City mwaka 2009 na baadae Moyes aliondoka baada ya kuajiriwa na Man utd mwaka 2013.
Lescot amekubali kujiunga na The Black Cats, baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu, kufuatia mkataba wake na klabu ya AEK Athens kuvunjwa mwezi Novemba mwaka jana.
Amesaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Sunderland hadi mwishoni mwa msimu huu.
Lescott alikua sehemu ya kikosi cha klabu ya Aston Villa msimu uliopita, na kwa bahati mbaya alishindwa kushirikiana na wenzake, na kujikuta wakiishusha daraja kwa mara ya kwanza klabu hiyo ya mjini Birmingham.
Pia amewahi kuzitumikia klabu nyingine za nchini England kama Wolverhampton Wanderers, Everton, Manchester City na West Bromwich Albion.
Klabu ya Sunderland kwa sasa inaburuza mkia wa msimamo wa ligi ya nchini England kwa kuwa na point 15.