Timu ya Njombe Mji ya mkoani Njombe imepata ushindi wa kwanza kwenye uwanja wake wa nyumbani tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0.
Katika mchezo huo uliopigwa dimba la Sabasaba Mjini Njombe, Njombe ilionekana kuimarika na kutawala mchezo tofauti na michezo mingine iliyopita huku ikifanya mashambulizi mengi zaidi ya Kagera Sugar.
Bao pekee la Njombe Mji limefungwa na Ditram Nchimbi dakika ya 76 ya mchezo kwa njia ya penati baada ya beki wa Kagera Mohamed Fakhi kumfanyia madhambi mchezaji wa Njombe Mji katika eneo la hatari.
Kwa matokeo hayo Njombe Mji imepanda hadi nafasi ya 14 ikiwa na pointi 11 katika michezo 13 iliyocheza hadi sasa wakati Kagera ikiwa nafasi ya 9 na pointi 12 katika michezo 13.