Mlinda mlango wa klabu ya Everton Jordan Pickford, amekabidhiwa jukumu la kuwa mlinda mlango wa kikosi cha kwanza cha England kitakacho shiriki fainali za kombe la dunia mwaka huu 2018.
Pickford, amekabidhiwa jukumu hili baada ya kutangazwa kwa kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 cha taifa hilo, ambacho kitapambana kwenye fainali hizo nchini Urusi, ili kufikikia lengo la kutwaa ubingwa wa dunia.
Kocha mkuu wa England Gareth Southgate, amesema naamini uwezo wa mlinda mlango huyo ambaye atakaesaidiwa na wenzake Jack Butland (Jezi namba 13) na Nick Pope (Jezi namba 23).
Pickford atavaa jezi namba moja, huku akikumbukwa kufanya vizuri katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Nigeria mwishoni mwa juma lililopita jijini London, japo aliruhusu bao katika mchezo huo ambao England walishinda mabao mawili kwa moja.
Nahodha mpya wa kikosi cha England Harry Kane, atavaa jezi namba 9, tofauti na alivyozoeleka anapokua kwenye kikosi cha klabu ya Tottenham ambapo huvaa jezi namba 10.
Mshambuliaji wa Man City Raheem Sterling, atavaa jezi namba 10, huku Dele Alli akiendelea na jezi namba 20 ambayo pia huitumia kwenye klabu yake ya Spurs.
Ingizo jipya kwenye kikosi cha England Trent-Alexander Arnold atavaa jezi namba 22, huku akitarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha England katika mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Costa Rica, siku ya Alhamis.
England wataanza kampeni ya kusaka ubingwa wa dunia kwa kucheza dhidi ya Tunisia Juni 18 mjini Volgograd.
Kikosi cha mwisho cha England kilichotangazwa na kocha Gareth Southgate na namba zao za jezi:
- Jordan Pickford, 2. Kyle Walker, 3. Danny Rose, 4. Eric Dier, 5. John Stones, 6. Harry Maguire, 7. Jesse Lingard, 8. Jordan Henderson, 9. Harry Kane, 10. Raheem Sterling, 11. Jamie Vardy, 12. Kieran Trippier, 13. Jack Butland, 14. Danny Welbeck, 15. Gary Cahill, 16. Phil Jones, 17. Fabian Delph, 18. Ashley Young, 19. Marcus Rashford, 20. Dele Alli, 21. Ruben Loftus-Cheek, 22. Trent Alexander-Arnold na 23. Nick Pope