Beki wa pembeni wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Jordi Alba, atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa majuma mawili ama zaidi, kufuatia majeraha ya misuli ya paja aliyoyapata akiwa kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa hatua ya makundi, ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund usiku wa kuamkia leo.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 30, alilazimika kutolewa nje ya uwanja dakika ya 40 ya mchezo huo uliounguruma nchini Ujerumani, na nafasi yake kuchukuliwa na Sergi Roberto.
Taarifa iliyotolewa kupitia tovuti ya klabu ya FC Barcelona imeeleza kuwa, beki huyo ataanza kufanyiwa matibabu mara moja, baada ya kuwasili mjini Barcelona.
Kwa mantiki hiyo Alba atakosa mchezo wa ligi ya Hispania dhidi ya Granada utakaochezwa mwishoni mwa juma hili, kisha Villarreal na Getafe.
Huenda akarejea tena uwanjani katika mchezo wa mzunguuko wa pili wa ligi ya mabingwa Ulaya, ambapo FC Barcelona watakua nyumbani wakiwakaribisha Inter Milan ya Italia, Oktoba 02.
Kuumia kwa Alba, huenda kukatoa nafasi ya kuanza kuonekana kwa beki wa pembeni Junior Firpo, aliesajiliwa wakati wa usajili wa majira ya kiangazi akitokea Real Betis, kwa ada ya Euro milioni 18, sawa na dola za kimarekani milioni 19.88.