Kiungo kutoka nchini Italia Jorge Luiz Frello Filho (Jorginho) amewataka wachezaji wa Chelsea kupambana kufa na kupona kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, hatua ya 16 bora dhidi ya mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich, utakaochezwa baadae hii leo.
Jorginho mzaliwa wa Brazil ametoa wito huo kwa wachezaji wenzake, huku akibainisha kuwa, endapo watajitoa kwa asilimia zote watakua na kila sababu ya kushinda mchezo huo, utakaounguruma jijini London.
Chelsea wamekua na matoko ya kutoridhisha wanapocheza nyumbani msimu huu, kwani katika michezo 14 wameshinda michezo sita, hali ambayo imechukuliwa kama kichocheo cha kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kutoa msisitizo kwa wachezaji wenzake.
Kwa mara ya mwisho Chelsea walicheza nyumbani mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Totenham Hotspurs, na kupata ushindi wa maboa mawili kwa moja.
Jorginho ameongeza kuwa, kila mchezaji anapaswa kupambana bila kuchoka, huku akitumainia matokeo mazuri ambayo yatawawezesha kwenda mjini Munich wakiwa na matumaini ya kusonga mbele katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
“Tuna michezo miwili ambayo inapaswa kutoa nafasi kwetu ili tufanikishe lengo la kusonga mbele kwenye michuano hii, njia rahisi ni kila mmoja wetu kutambua umuhimu wa mchezo wetu dhidi Bayern Munich,” amesema Jorginho.
“Tunapaswa kucheza kwa ushirikiano mkubwa, tukiwakabili wapinzani wetu na kuwashambulia kwa namna yoyote ile, lengo ni kupata matokeo mazuri katika uwanja wetu wa nyumbani, kabla ya kwenda ugenini.”
“Kila mmoja wetu anastahili kupambana bila kuchoka, ninaamini tukiingia uwanjani kwa ari ya namna hii, tutashinda.”
Chelsea wanakwenda kupambana, huku ikikumbukwa waliwahi kuwafunga Bayern Munich kwenye mchezo wa fainali mwaka 2012, kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Mchezo wa mkondo wa pili wa wababe hao umepangwa kuchezwa Machi 18.
Mchezo mwingine ya ligi ya mabingwa barani Ulaya utakayochezwa leo jumanne utakua kati ya Società Sportiva Calcio Napoli dhidi ya mabingwa wa Hispania FC Barcelona.