Meneja wa Klabu ya AS Roma ya Italia, Jose Mourinho anakabiliwa na rungu la Shirikisho la Soka Barani Ulaya ‘UEFA’ kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu alivyofanya kwa mwamuzi Anthony Taylor wakati na baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Europa League ambao timu yake ilipoteza mbele ya Sevilla, Jumatano (Mei 31) jijini Budapest, Hungery.
Wakati mchezo unaendelea, Taylor alimuonyesha kadi ya njano Meneja huyo kutokana na kuonyesha utovu wa nidhamu kwenye benchi na katika hali ya kushangaza, Mourinho alimshambulia kwa maneno ya kashfa mwamuzi huyo katika eneo la kuegeshea magari kwenye Uwanja wa Puskas, wakati alipokuwa akitoka uwanjani hapo.
Na sasa inaripotiwa kwamba UEFA tayari imeshawasilisha mashtaka yake mbele ya kamati ya usimamizi, maadili na nidhamu ikimtuhumu Mourinho kwa utovu wa nidhamu kutokana na kile alichokionyesha Jumatano (Mei 31).
Iwapo kamati hiyo itamkuta na hatia, Meneja huyo wa zamani wa Chelsea, Real Madrid na Manchester United adhabu ambazo anaweza kukumbana nayo ni kufungiwa na kupigwa faini.
Lakini mashtaka hayo hayajamhusu Mourinho peke yake bali pia hata klabu zote mbili zilizocheza fainali hiyo zimewekwa kikaangoni kutokana na kushindwa kudhibiti wachezaji na mashabiki wao kweye mechi hiyo.
Kuthibitisha kukithiri kwa utovu wa nidhamu kwenye mechi hiyo, idadi ya kadi 13 za njano zilitolewa na Refa Taylor kwa pande hizo mbili huku saba kati ya hizo zikienda kwa AS Roma.
Katika mechi hiyo, Sevilla walitwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 120 za mchezo.