Imeelezwa kuwa Meneja wa AS Roma ya Italia Jose Mourinho ameikataa ofa ya kurudi kuinoa Chelsea baada ya kufuatwa na bilionea na mmiliki wa miamba hiyo ya Stamford Bridge, baada ya kumfuta kazi Graham Potter mwezi uliopita.
Bilionea Todd Boehly, alimfuata Mourinho nchini Italia na kumtaka arudi kukinoa kikosi cha The Blues, lakini Meneja huyo kutoka nchini Ureno alikataa kwa kusisitiza hayupo tayari kurudi jijini London kwa sasa.
Kwa sasa, Mourinho mwenye umri wa miaka 60, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake AS Roma, huku akiwa ameiongoza timu hiyo kwenye ubingwa wa Europa Conference League msimu uliopita.
AS Roma hawapo vizuri sana kwenye ligi msimu huu na kwa sasa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Serie-A lakini wamefanikiwa kutinga nusu fainali ya Europa League Meneja huyo anayejitambulisha kama The Special One.
Kinachoelezwa, Mourinho aligomea ofa ya kwenda kuwa kocha wa Chelsea msimu ujao kutokana na timu hiyo kwa sasa kuwa kwenye msako wa Meneja mpya.
Chelsea kwa sasa ipo chini ya Meneja wa muda, Frank Lampard ambaye ataifanya kazi hiyo hadi mwishoni wa msimu huu 2022/23.
The Blues ilimweka Mourinho kwenye orodha ya Mameneja inayowahitaji, lakini bosi huyo wa zamani wa FC Porto, Manchester United, Inter Milan na Real Madrid aligomea ofa hiyo na kusema hayupo tayari kurudi kwenye klabu hiyo ya London Magharibi.