Muamuzi Gianluca Rocchi kutoka nchini Italia amemkera meneja wa Man Utd Jose Mourinho, ambaye usiku wa kuakia leo alikishuhudia kikosi chake kikishindwa kujipapatua dhidi ya mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid katika mchezo wa European Super Cup.
Katika mchezo huo ambao uliashiria kufunguliwa rasmi kwa michuano ya barani Ulaya msimu wa 2017/18, Man Utd walikubali kuchapwa mabao mawili kwa moja.
Mourinho aliwaambia waandishi wa habari kuwa, muamuzi Rocchi alishindwa kuheshimu mchezo kwa asilimia 100, na badala yake alionyesha mapenzi dhahir kwa wapinzani wa Real Madrid kwa kumsikiliza Ronaldo alichokua anakihitaji.
Alisema muamuzi huyo mwenye umri wa miaka 43, alimlinda kwa makusudi Cristiano Ronaldo, pale alipofanya makosa na wakati mwingine alipoonyeshwa upinzani na wachezaji wa Man Utd, jambo ambalo anaamini halikua sahihi kutokana na wachezaji wote waliokuwepo uwanjani kuwa na hadhi sawa.
“Ilionekana dhahir Ronaldo alikua analindwa, hata alipokwenda kulalamika kwa muamuzi alisikilizwa, sikubaliani na hili hata kidogo, na ninaamini kulikua na makusudi yaliyodhamiria kufanywa na Rocchi.
“Cristiano Ronaldo kweli ni mchezaji wenye sifa za kipekee katika kipindi hiki, lakini haipaswi kwa muamuzi kuvuka mipaka na kumuona ana hadhi kubwa ya kusikilizwa na kulindwa kuliko wachezjai wengine.”
Pamoja na kumtaja mchezaji huyo kwa kusema alilindwa na muamuzi kwa makusudi, bado Mourinho alionekana kuwa na mahusiano mazuri na Ronaldo, hasa walipoonekana wakiongea wakati wa mapumziko ya mchezo huo.