Kocha Mkuu wa AS Roma, Jose Mourinho, amesema anatarajia kufanya kazi nchini Saudi Arabia siku moja baada ya mwenzake, nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo, kuongoza kwa kujiunga na Al Nassr, huku wachezaji wengi wakijiunga na timu za Ligi Kuu ya nchi hiyo, Saudi Pro League.
Mourinho alionekana kujiamini kuhamia Saudi Arabia wakati wa mahojiano na Kituo cha Televisheni cha MBC cha Misri, kinachomilikiwa na Saudi MBC Group.
“Nitaenda Saudi Arabia katika muda wa mapumziko, lakini nina hakika kwamba nitafanya kazi huko. Sijui ni lini, lakini nina uhakika wa hilo,” alisema Mourinho, ambaye yuko kwenye shinikizo baada ya kuanza vibaya msimu huu pale AS Roma.
“Hakuna anayejua siku zijazo, lakini kwa hakika nitafanya kazi Saudi Arabia.” Mourinho mwenye umri wa miaka 60, alisema hivi karibu alikataa ofa kubwa kutoka Saudi Arabia ili abaki AS Roma kwa msimu watatu baada ya kuiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Uefa Conference League na kutinga fainali ya Ligi ya Europa, lakini Julai iliyopita pia alijiunga na bodi ya wakurugenzi ya Mahd Academy ambayo inashughulikia ugunduzi wa vipaji nchini Saudi Arabia.