Kocha Mkuu wa AS Roma Jose Mourinho amesisitiza bao la Romelu Lakaku sio muhimu baada ya Mshambuliaji huyo kufunga katika dakika ya 82 kwenye ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Empoli.
Lukaku alifunga bao lake kwanza akiwa na uzi wa Roma baada ya kusajiliwa akitokea Chelsea kwa mkopo lakini kocha wake alionyesha kutokuwa na mhemuko.
Licha ya kulipuuza bao hilo, Mourinho alimsifu Lukaku kwamba alibadilisha upepo kufuatia ushindi huo mkubwa baada ya kuanza msimu kwa kusuasua.
“Bao lake halikuwa muhimu. Inaweza kuwa muhimu kwake, najua Washambuliaji wanaishi kwa sababu ya mabao.” alisema Mourinho.
“Tangu alipowasili amekuwa kila kitu kwenye timu, haijalishi kama akifunga au hakufunga.
“Ni wazi atajisikia furaha baada ya kufunga bao kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yake, Lukaku ameleta utofauti kwenye timu na bado tunahiji kujifunza jinsi gani ya kucheza naye, Lukaku anahitaji kufurahi na mashabiki pia wanamkubali.” aliongeza.
Lukaku alianza mechi yake ya kwanza ya Serie A baada ya Mourinho kuamua kumuweka benchi Andrea Belotti na kurudisha matumaini kwa mashabiki baada ya kuanza kwa kusuasua Serie A.
Katika mechi hiyo mshambuliaji wa zamani wa Juventus, Paulo Dybala alicheka na nyavu mara mbili katika dakika ya pili na 55, bao la tatu likiwekwa kimiani na Renato Sanches, jingine la kujifunga likitupiwa na mchezaji wa Empoli, Alberto Grassi dakika ya 35, Bryan Cristante alifunga dakika ya 79, na Gianluca Mancini alifunga dakika ya 86.