Kocha Mkuu wa AS Roma Jose Mourinho anaweza kufungiwa baada ya matamshi yake ya kutatanisha kuhusu Mwamuzi Matteo Marcenaro kabla ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sassuolo mwishoni mwa juma lililopita.

Vijana wa Mourinho walitoka nyuma na kuifunga Sassuolo ikiwa pungufu hata hivyo maneno mengi yaliibuka kabla ya mchezo huo wa Serie A.

Kabla ya mechi, Mourinho alikiri kwamba alikuwa hana imani na Mwamuzi Marcenaro ambaye alipangwa kwa ajili ya mchezo huo.

“Kusema kweli, nitasema kwamba nina wasiwasi kuhusu mwamuzi,” alisema kocha huyo kutoka nchini Ureno, katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kabla ya mchezo huo wa mwishoni mwa juma lililopita.

“Mwamuzi huyo amechezesha mechi zetu mara tatu, sidhani kama ana utulivu wa kufanya kazi kwa ngazi ya juu kabisa.”

Shirikisho la Soka Italia (FIGC) lilianzisha uchunguzi kuhusu matamshi ya Mourinho kwani aliitwa na Mwendesha Mashtaka, Giuseppe Chine, Ijumaa (Desemba 08) ili kutoa utetezi wake, kama ilivyoripotiwa na Gazzetta dello Sport.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mourinho alishirikiana na FIGC wakati wa mkutano huo uliodumu kwa muda wa dakika 90, hata hivyo huenda akasimimaishwa kwa muda wa siku 10.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Manchester United na Tottenham huenda akakosa mechi moja ya Serie A, huku AS Roma ikitarajiwa kuikaribisha Fiorentina Jumapili (Desemba 17).

Singida FG yakutana na rungu lingine FIFA
Vifaa Tiba, Noti bandia vyadakwa Njombe