Baada ya bao la ugenini kukisaidia kikosi chake katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya nusu fainali ya kombe la ligi nchini England (EFL Cup), meneja wa Man Utd Jose Mourinho ametoa kauli ya kustaajabisha.

Mourinho ambaye alikishuhudia kikosi chake kikiambulia kisago cha mabao mawili kwa moja dhidi ya Hull City usiku wa kuamkia hii leo, aliwaambia waandishi wa habari hawapoteza mchezo huo.

Mourinho alizungumza kauli hiyo kwa kujiamini, na alitoa sababu ya kusema hivyo, huku akiegemea katika faida ya bao la ugenini ambalo limewapitisha na kutinga kwenye hatua ya fainali.

Alisema huenda kuna baadhi ya mashabiki wakashangazwa na alichokizungumza, lakini kwa ujumla hawezi kubadilisha kauli hiyo kutokana na kikosi chake kujidai na ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa mawili.

Katika mchezo huo ambapo Hull City walikua nyumbani, walitangulia kupata bao la kuongoza kwa njia ya mkwaju wa penati iliyopigwa na Tom Huddlestone katika dakika ya 35, lakini dakika ya 66 Paul Pogba aliisawazishia Man Utd.

Baye Oumar Niasse aliifungia Hull City bao la pili na la ushindi, japo haliwakusaidia kutokana na matokeo yaliyopatikana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, ambapo Man Utd walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Man Utd watakutana na Southampton katika mchezo wa hatua ya fainali ya michuano ya kombe la ligi (EFL Cup), ulipangwa kuchezwa Februari 26 kwenye uwanja wa Wembley.

Southampton wametinga hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa kuifunga Liverpool jumla ya mabao mawili kwa sifuri.

Cristiano Ronaldo: Msinishindanishe Na Lionel Messi
Vanessa aitaja Simu chanzo cha kugombana na Jux