Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku ametoa maoni yake kuhusu kinachopaswa kufanyika Zanzibar kufutia sintofahamu iliyoibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, na kutangaza marudio ya uchaguzi huo Machi 20 mwaka huu.

Akiongea na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), Butiku alieleza kuwa haki itendeke Zanzibar kwani kilichofanyika bado kimeacha maswali mengi ingawa waliotoa tangazo hilo wanaweza kuwa hawakukosea.

“Nasema kwa kusisitiza haki itendeke Zanzibar kwa sababu misingi ya Taifa letu tangu uhuru na Mapinduzi Mtukufu ni haki, amani na umoja. Mimi napenda kuamini kuwa siku ya uchaguzi Wazanzibar waliamua jambo na uamuzi wao ndio ambao mpaka sasa hatujapata maelezo ya kutosha kwanini hapo katikati walisema ulikosewa,” alisema Butiku.

“Naamini Wazanzibari wangetendewa haki angalau uamuzi walioufanya ujulikane kwao wote na sisi,” aliongeza.

Alieleza kuwa ana imani Rais John Magufuli amezungumza na pande zote mbili na kwa pamoja wanaweza kupata jibu.

 

Bunge kuanza mchakamchaka leo, haya ni mambo 7 yatakayowasha moto
Mbunge atimuliwa kwenye kikao na Polisi