Beki kutoka nchini Croatia na klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani, Josko Gvardiol, anawindwa na Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City.
Mpango wa usajili wa Beki huyo, unetarajiwa kukamilishwa endapo Aymeric Laporte ataondoka msimu huu wa majira ya joto, kwa mujibu wa ESPN.
Gvardiol yuko kwenye orodha fupi ya wachezaji wa kuchukua nafasi ya Laporte, ambaye yuko tayari kuondoka pale kwenye dimba la Etihad.
RB Leipzig tayari imempoteza Christopher Nkunku aliyetua Chelsea na Konrad Laimer kwenda Bayern Munich msimu huu wa majira ya joto na ingependelea kumbakiza Gvardiol kwa angalau mwaka mmoja zaidi.
Vyanzo vimeiambia ESPN kwamba RB Leipzig inaweza kuomba ada ya uhamisho ya juu kama euro milioni 100 kwa sababu Gvardiol mwenye umri wa miaka 21, alisaini mkataba mpya Septemba 2022 na yuko chini ya mkataba hadi 2027.
Laporte anatathmini chaguzi zake kabla ya uwezekano wa kuondoka City na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, alikosa namba mbele ya Ruben Dias, John Stones, Manuel Akanji na Nathan Ake msimu uliopita na alicheza mechi 12 pekee kwenye Ligi Kuu England.
Laporte ana mkataba pale Etihad hadi 2025 na City wataomba ada kubwa kabla ya kumruhusu kuondoka.
Wakati huo huo, vyanzo viliiambia ESPN kwamba kiungo wa kati wa City, Bernardo Silva ana ofa kutoka kwa klabu ya Saudi Arabia, Al Hilal.