Joto la kuwachuja makada 38 wa CCM linaloendelea kupanda jijini Dodoma limeambatana na tetesi za matukio kadhaa ikiwa ni pamoja na wapambe wa baadhi ya wagombea kudaiwa kutaka kuwakodisha watunisha misuli kufanya fujo endapo jina lao litakatwa.

Akizungumza na Star TV, mtu mmoja aliyetambulishwa kama kiongozi wa mabaunsa wa jiji la Mwanza alieleza kuwa alishawishiwa na kada wa chama hicho aitwae Mtemi Yeredi kuwa awakusanye baadhi ya mabaunsa kwa ajili ya kwenda jijini Dodoma kufanya fujo endapo jina la mgombea wao halitapitishwa.

Kiongozi huyo wa mabaunsa alieleza kuwa aliikataa ofa hiyo baada ya kutafakari madhara ya kufanya fujo katika mji huo na sababu za kufanya hivyo.

Star TV iliongea pia na Mtemi Yeredi kwa njia ya simu ambapo alikanusha taarifa hizo kwa madai kuwa hakuwahi kumfuata wala kumshawishi mtu yoyote kwenda Dodoma kufanya fujo.

Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, juzi alieleza msimamo wa chama hicho kuwa hakitafanya uchaguzi kwa shinikizo na presha ya wapambe wa wagombea nafasi ya kuwania kiti cha urais.

Idadi kubwa ya wafuasi wa CCM imefurika mjini Dodoma huku mbivu na mbichi zikitarajiwa kufahamika ndani ya muda wa siku 5. Majina matano yatachujwa kutoka kwenye majina 38 ya watia nia waliorudisha fomu za wadhamini, kisha kupata majina matatu kati ya matano na hatimaye kulitoa jina moja.

Mchumba wa Luteni Karama Amshukia Inspector Haroun
Tundu Lissu aizungumzia Barua ya Shibuda Kwa Chadema