Joyce Banda, aliyekuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Malawi ametangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Mwanasiasa huyo ambaye aliachia kiti cha urais baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2014, ameamua kumuunga mkono mgombea wa chama cha upinzani cha Malawi Congress Party, Lazarus Chakwera.
Awali, Banda aliyekuwa amekimbilia nje ya nchi baada ya kushindwa uchaguzi kwa kile kinachoaminika na wengi kuwa ni kutokana na kuandamwa na kashfa ya ufisadi wa mabilioni inayofahamika kama ‘Cashgate scandal’, alirejea nchini na kuendeleza harakati za kisiasa akiongoza chama cha People’s Party.
Kupitia taarifa ya pamoja ya Banda na Chakwera, wawili hao wameeleza kuwa walikuwa wamezungumzia kuunganisha nguvu tangu mwaka 2015 baada ya uchaguzi uliomuondoa mwanasiasa huyo madarakani.
“Malawi ni kubwa zaidi ya mtu mmoja. Hivyo tumeamua kuweka pembeni mambo ya mmoja-mmoja na kujikita katika mambo ambayo ni muhimu maslahi mapana ya taifa letu,” imeeleza taarifa hiyo ya pamoja.
Banda ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 68, alichaguliwa kuwa rais wa Malawi Aprili 2012 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bingu wa Mutharika. Wakati huo, Banda alikuwa Makamu wa Rais, hivyo baada ya kuchaguliwa aliongoza nchi hiyo hadi Mei 2014 aliposhindwa katika uchaguzi mkuu.