Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kuwapokonya wale wote walioshindwa kuviendeleza viwanda vyao.
Ametoa agizo hilo mapema hii leo Chalinze mkoani Pwani alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kusindika matunda cha Sayona kilichopo mboga Chalinze, amesema kuwa kwa yeyote aliyeshindwa kukiendeleza anyang’anywe na kama akikaidi achukuliwe hatua kali.
Amesema kuwa vipo viwanda 197 nchini ambavyo vimekufa na vingine vimegeuzwa kuwa magodauni na kufugiwa mbuzi hivyo ni vyema viwanda hivyo vikafufuliwa ili kuinua uchumi wa nchi.
“Kiwanda sio mwanamwali wa kuweka ndani, vinatakiwa vifanyekazi, waziri nakuagiza wale wote walioshindwa kuviendeleza wanyang’anye, wakikaidi waweke ndani ili wakitoka huko wakute mambo yameshabadilika, na hiki ndicho kitakuwa kipimo chako cha kazi,”amesema Rais Dkt. Magufuli.
Aidha, ameongeza kuwa watu hao walipewa viwanda kwa bei chee lakini walivitelekeza, hivyo amemtaka Mwijage kutopata kigugumizi wala kumuangalia mtu usoni na atakaegoma akamatwe na kuwekwa ndani.
Hata hivyo, Rais Magufuli amempongeza mwekezaji Subhash Patel kwa kutoa mitambo tisa ya kusogeza maji kwa Mamlaka ya maji Chalinze-CHALIWASA, iliyochukuwa milioni 100.