Rais Dk. John Pombe Magufuli leo Septemba 14, 2016 amemuapisha Dk. Ramadhani Kiwana Dau kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.

Taarifa ya Ikulu iliyosambaza jana, ilisema Dk. Dau aliyeteuliwa Februari 15, 2016, anakwenda kujaza nafasi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania, Malaysia, Dk. Aziz Ponary Mlima ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi, Dk. Dau alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Rais Dk. Magufuli pia amewaapisha Makatibu Tawala wa mikoa mitatu aliowateuwa hivi karibuni ambao ni Bw. Eliya Ntininga Ntandu anayekuwa Katibu Tawala wa kwanza Mkoa wa Songwe ulioanzishwa rasmi Februari 2016, Bw. Ado Stephen Mapunda anayekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mara, anayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw, Benedict ole Kuyan aliyestaafu. Mwingine aliyeapishwa ni Bw Tixon Tuliangine Nzunda anayekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa.

Baaada ya kuapishwa Dk. Dau na Makatibu wote walikula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili,  Jaji Salome Kaganda wakishuhudiwa na Rais Dk. Magufuli.

David Moyes Aufyata, Kufanya Kazi Na Lamine Kone
Wanafunzi wamng’oa meno mwalimu, wamtuhumu kuwadhalilisha