Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewasamehe jumla ya wafungwa 3,973, siku moja kabla ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 56 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, kati ya wafungwa hao 3,717 wamesamehewa vifungo vyao na 256 waliokuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa hadi kufa wamebadilishiwa adhabu hiyo.
“Mhe. Rais Magufuli amesema ana matumaini kuwa wafungwa hao wamejifunza na wamejirekebisha ili waungane na jamii katika kulitumikia Taifa wakiwa raia wema wanaozingatia sheria na taratibu,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuitumia siku ya kesho (Aprili 26, 2020) kutafakari Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Rais ametoa wito pia kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona (covid-19) ikiwa ni pamoja na kujiepusha na mikusanyiko na safari zisizo za lazima; na kumuomba Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na janga hilo.