Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa amefanya uchunguzi na kubaini mchezo mchafu katika vipimo vya virusi vya corona, vilivyofanywa na Maabara Kuu ya Taifa (National Referral Laboratory).
Akizungumza leo, Mei 3, 2020 katika hafla ya kumuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Rais Magufuli amesema kuwa baada ya kuona majibu mengi ya vipimo vya sampuli za watu yanaonesha wameathirika, aliamua kufanya uchunguzi wa siri kwa kutumia vyombo vya usalama na timu maalum ya wataalam aliowateua.
Rais alisema kuwa timu hiyo iliwasilisha sampuli za vitu mbalimbali ambavyo sio binadamu na kuvipa majina ya binadamu ili kubaini kinachoendelea. Baadhi ya vitu hivyo ni pamoja na papai, fenesi, kware, mbuzi vilikutwa na virusi vya corona.
“Sample ya oili ya gari kwa mfano tuliipa jina la Jabir Hamza mwenye miaka 30 (mwanaume), ile ilileta negative (haikuwa na maambukizi), tulipopeleka sample ya fenesi ambayo tuliipa jina la Sara Samweli mwenye miaka 45 (mwanamke), matokeo yake yalikuwa ‘inconclusive’. Tulipopeleka sample ya papai, tukaipa jina la Elizabeth Anne miaka 26 (mwanamke), papai lile lilikuwa positive… kwamba lina corona. Maana yake maji yaliyotolewa mle kwenye papai ni positive (yameathirika),” amesema Rais Magufuli.
“Tulipeleka sample ya ndege kware imekuwa positive, tumechukua mbuzi akawa positive, tukachukua kondoo akawa negative, n.k,” aliongeza.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli amesema kuwa kuna tatizo katika masuala ya vipimo vya corona akitilia shaka vifaa vinavyotumika.
“Huenda hizi mashine za vipimo, zimeweka zikipima vipimo kadhaa inayofuata lazima iwe positive. Hili nalo lazima liangaliwe. Nilishasema tusikubali kila msaada tukafikiri ni kwa faida ya nchi. Na ndio maana wengi wanaoambiwa wana corona ni wazima tu wala hawasikii kitu kingine. Of course mnaweza kusema labda kinga zao za mwili ziko juu, ni sawa… lakini haya yote tuyaangalie,” ameongeza.
Alitoa wito kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi za Afrika kuchukua hatua na kuliangalia suala hili kwa undani; na pia kufanya majaribio kwa vitu vingine ili wabaini kile alichokibaini.
“Natoa wito kwa wenzangu Afrika, wachukue sampuli ya kitu chochote kile, hata ya ukuta, hata ya mjusi au kitu chochote, watakuja kukuta haya ninayoyazungumza. Mimi ni mwanasayansi najua ninachokizungumza, na hii kazi imefanywa na watu wenye uwezo,” alisema.
Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi na kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona, akieleza kuwa ugonjwa huu utapita kama magonjwa mengine.
Alisema kuwa anafikiria kutoa ruhusa ya kufunguliwa kwa Ligi za michezo mbalimbali, kwakuwa inaonekana watu wanaoshiriki michezo na kufanya mazoezi hawaathiriki zaidi na ugonjwa huu.
Na hizi siku za mbeleni nafikiria kuruhusu hata Ligi ziendelee ili watu wawe wanacheza na wengine wanaangalia kwenye TV, tuweke utaratibu mzuri. Hata kwa wanamichezo sijaona anayedhurika sana, hii inawezekana kwa wanaofanya michezo corona inawakwepa,” alisema Rais Magufuli na kusisitiza kuwa hatafunga mikoa ya Dar es Salaam na Tanga kama wanavyotaka baadhi ya watu.
Aliwataka pia wanasiasa kutotumia ugonjwa huu kama mtaji wa kisiasa kwani hautawasaidia.
Siku ya uhuru wa vyombo vya habari: EU wakemea vizuizi kipindi cha Corona
Viongozi wa Dini Morogoro waungana na serikali kupambana na Corona