Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa UN itaimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika kutekeleza majukumu mbalimbali, hususan tatizo la wakimbizi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ambapo amesema Guterres alikutana na Rais Magufuli kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), unaoendelea mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Guterres ameahidi kuwa UN itaongeza ushirikiano na Tanzania na kwamba itaweka msisitizo zaidi katika kukuza wadau mbalimbali wa maendeleo ndani ya jumuiya ya kimataifa, kuchangia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuwapa hifadhi wakimbizi wa nchi mbalimbali tangu mwaka 1971.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amempongeza Guterres kwa kuchaguliwa kwake hivi karibuni kushika wadhifa huo.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa na kumwelezea juhudi mbalimbali, zinazofanywa na Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushughulikia mgogoro wa Burundi chini ya Mpatanishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na alimhakikishia kuwa juhudi hizo zinakwenda vizuri.