Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wanajeshi hao wameuawa katika operesheni ya ulinzi wa amani katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aidha, Rais Dkt. Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wa wote JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.

“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC,” amesema Rais Dkt. Magufuli

Hata, hivyo Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tukio hilo, na pia amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida

 

 

Israel yaifyatulia Palestina Makombora
Magazeti ya Tanzania leo Desemba 9, 2017