Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo vya wafanyakazi 5 wa vyombo vya habari vya Azam Media Limited vilivyotokea leo tarehe 08 Julai, 2019 katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 2:30 asubuhi katika eneo la Kizonzo, katikati ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida) ambapo basi aina ya Coaster lililowabeba wafanyakazi wa Azam Media Limited likielekea Mwanza limegongana uso kwa uso na Lori la mizigo lililokuwa linakwenda Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Azam Media Limited walikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea kwenye sherehe za uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya sherehe hizo.
Aidha, katika salamu hizo, Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na taarifa na ajali iliyosababisha vifo vya watu 7 wakiwemo wafanyakazi hao 5, Dereva na Msaidizi wake na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi.
“Nimeshtushwa sana na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndg. Said Salim Bakhresa, ndugu wa Marehemu wote, Mtendaji Mkuu Ndg. Tido Mhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari wote na watu wote walioguswa na vifo hivi” amesema Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli amewaombea majeruhi 3 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Vile vile Rais Magufuli amerejea wito wake wa kuwataka watumiaji wa barabara hususani madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.