Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli Dkt. John Magufuli amewaapisha Mawaziri 21 aliowateua hivi karibuni.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo Desemba 9, 2020 Ikulu, Chamwino jijini Dodoma Rais Magufuli pia amewaapisha Manaibu Waziri aliowateua pamoja na Mawaziri hao wiki iliyopita.
Akizungumza mara baada ya zoezi la kuwaapisha Mawaziri hao pamoja na Manaibu wao, Rais Magufuli amewataka wateule wote kwenda kufanya maamuzi kwa maslahi ya taifa ili kusaidia kuondoa shida za wananchi.
“Nawaomba Mawaziri na Naibu Mawaziri mkafanye maamuzi, ni nafuu ukafanye uamuzi mbaya kuliko kutokufanya uamuzi kwa sababu tatizo letu jingine tulilonalo unashindwa kutoa uamuzi kwa sababu hutaki kuonekana mbaya. Kafanyeni uamuzi hasa unaohusu maslahi ya taifa,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameeleza kuwa katika uteuzi alioufanya licha ya ugumu alioupitia ameweka uwiano kwa kuwachagua vijana na wazee huku akiweka bayana sababu ya kumchagua Kapteni Mstaafu George Mkuchika kuwa Waziri wa Utumishi.
“Nimemchagua Mkuchika kwa sababu baraza la mawaziri linahitaji wazee, tumebalance wazee na vijana, kuna (George) Mkuchika amekuwamo wakati wa Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Hata mimi kwenye baraza nataka wazee na lazima tuzitunze hazina zetu” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Elimu kuanzisha somo la historia ya Tanzania kuwa la lazima kwa wanafunzi.