Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameruhusu kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) baada ya kufurahishwa na kazi nzuri waliyoifanya, akiirejea pia hatua yake ya kutopandisha mishahara ya wafanyakazi kwa mwaka huu.
Ametoa agizo hilo leo alipokuwa akihutubia katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, akipokea gawio la Serikali la sh. 1.5 bilioni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15 kutoka TTCL.
Rais Magufuli alisema kuwa amefurahishwa na kazi nzuri iliyofanyika na kwamba anawaruhusu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kuamua kuhusu ongezeko la mishahara na stahiki za wafanyakazi wake.
“Wafanyakazi wanaofanya kazi kwa moyo, kwa utaalam, kwa uzalendo na kwa kuzalisha wana haki yote asilimia 100 kuongezewa mishahara yao na marupurupu yao. Kwa sababu wamepata kwa nguvu zao” amesema Rais Magufuli.
“Kwahiyo mheshimiwa Waziri na Bodi ya Wakurugenzi, mimi nikisikia siku moja mmezalisha zaidi na Serikali ikaongeza kupata dividend, mkaamua katika bodi yenu na katika menejimenti yetu… na kwasababu nilishasema mwaka huu hakuna kupandisha mishahara, lakini kwa ninyi mnaozalisha hivi hata mkipandisha mishahara ni safi tu,” ameongeza.
Aidha, Rais Magufuli ameutaka uongozi wa TTCL pamoja na wafanyakazi kutobweteka bali kuongeza bidii kwenye soko lenye ushindani mkubwa wa makampuni ya simu za mkononi nchini.
Amewataka pia kuangalia fursa akitoa mifano ya nchi nyingine za Afrika zilivyotumia teknolojia ya simu kutoa huduma inayowafanya wananchi kuweza kutambua ubora wa bidhaa wanazoagiza kwa njia ya mtandao.