Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka wafanyakazi wa Serikali kuwa wavumilivu kuhusu ahadi yake ya kupandisha mishahara kwani ataitekeleza kabla ya kuondoka madarakani kama alivyoeleza mwaka jana.
Kupitia hotuba yake kwa wafanyakazi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani maarufu kama Mei Mosi yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya, Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa ahadi yake bado anaikumbuka na anaendelea kufanyia kazi maombi ya makundi yote nchini.
“Katibu Mkuu wa TUCTA (Chama cha Wafanyakazi) amenikumbusha ahadi yangu ya mwaka jana kuwa kabla sijaondoka madarakani nitaongeza mishahara, lakini muelewe ndugu zangu bado niko madarakani,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, aliwataka wafanyakazi kuendelea kuvumilia na kushiriki katika kujenga uchumi wa nchi kwani hadi sasa mambo mengi yamefanyika na takwimu zinaonesha kuwa uchumi unakua kwa asilimia 7, kasi ambayo inaiweka Tanzania kuwa kati ya nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi. Aliongeza kuwa atakapopandisha mishahara atapandisha kwa kiwango kinachoridhisha kuliko kupandisha kiwango kidogo na kwamba hata akitangaza leo bei za bidhaa na huduma mbalimbali zitapanda ghafla.
Alisema kuwa zaidi ya watu laki moja na elfu kumi na nane (118,000) walipandishwa madaraja tangu mwaka 2015. Pia, watumishi wengi waliokuwa wanaidai Serikali wamelipwa madeni yao ambayo ni tofauti na mishahara ambayo yalikuwepo kwa takribani miaka kumi.
Aliongeza kuwa tangu alipoingia madarakani, Serikali imelipa madeni ya watumishi ikiwa ni pamoja na shilingi bilioni 9.5 zilizokuwa zinadaiwa na wastaafu.