Rais John Magufuli amewataka wakurugenzi wa Halmashauri ambao wanajihusisha na ulevi wa pombe kuacha mara moja na ‘kuokoka’.

Akizungumza leo katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya za Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa amepata taarifa kuhusu wakurugenzi wanaojihusisha na ulevi na kwamba wataondoka.

Amewataka wakurugenzi hao kubadilika kuanzia leo ili wasikutane na panga la kutumbuliwa nyadhifa zao.

“Wewe kama ulikuwa unajihusisha na ulevi, kuanzia leo ukirudi huko usikae hata karibu na pombe angalau uoneshe umebadilika, uokoke,” amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewataka viongozi wa ngazi zote za Serikali za mitaa kuvunja makundi yanayoibuka kati yao na kutengeneza uadui.

Amewataka wakurugenzi wavunje uadui na makundi yaliyojengeka kati yao na mameya au wenyeviti wa halmashauri, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na viongozi wengine wa kisiasa.

Amesema kuwa kuwepo kwa makundi na uadui unaojengeka kutokana na tofauti za kisiasa au ubinafsi wa kushindania madaraka kunadhoofisha juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi.

Hivyo, amewataka washikamane na kufanya kazi kwa umoja na kumaliza tofauti zao kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla. Amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili kwa uwazi changamoto zinazowakabili bila kujali tofauti zao za vyama vya siasa na kwamba ataufuatilia mjadala wao.

Nyumba ya mbunge Bobi Wine yashambuliwa kwa vilipuzi
Morata kusubiri hadi mwezi Novemba