Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo amezindua Mahakama inayotembea yenye vifaa vya kisasa yenye thamani ya Sh 470 milioni.
Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika leo katika maadhimisho ya siku ya sheria, kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewataka waendesha mashtaka kuhakikisha wanafanyia kazi tatizo la ucheleweshwaji wa upelelezi.
Rais Magufuli amesema kuwa ucheleweshwaji huo wa upelelezi ndio unaosababisha kesi kurundikana Mahakamani, akitoa mfano wa watu wanaokamatwa na vielelezo vya dawa za kulevya pamoja na meno ya tembo lakini hukaa rumande kwa muda mrefu kwa madai kuwa upelelezi unaendelea.
Akizungumza awali, afisa mwandamizi wa Mahakama alisema kuwa mahakama hiyo inayotembea itatumika kupokea kesi nyingi na kuzifanyia maamuzi katika ngazi ya chini. Alieleza kuwa kesi zinazowasilishwa mahakama ya mwanzo ni asilimia 68 ya kesi zote, hivyo gari hilo lenye mahakama litasaidia endeshaji wake kwa haraka.
Alisema kuwa Mahakama hiyo itakayofanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza itashughulika hasa na kesi za uvuvi haramu pamoja na kutoa elimu ya kisheria kwa umma.
Akizungumza katika siku hiyo, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alimshukuru Rais Magufuli kwa kuteua majaji wengi ambao wamesaidia juhudi za kuondoa mrundikano wa kesi mahakamani.
Jaji Mkuu pia alishauri sheria kuwekwa mitandaoni ikiwa ni pamoja na hukumu za mashauri ili Wananchi waweze kuzisoma na kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria.