Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuzindua rasmi hifadhi ya Taifa ya Burigi iliyopo wilayani Chato mkoani Geita siku ya Jumanne Julai 09 mwaka huu, hifadhi ambayo imepandishwa hadhi hivi karibuni kutoka lililokuwa pori la akiba la Burigi, ambapo pamoja na mambo mengine, atakabidhi vibali na hati kwa wawekezaji mbalimbali ili kuwekeza katika eneo hilo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao wanaokutana jijini Mwanza, ulioandaliwa na shirika la hifadhi za Taifa Tanapa, ukiwa na Kauli Mbiu ya Miaka 60 ya shirika hilo katika kuimarisha uhifadhi na kupanua wigo na fursa za Utalii kusini, Magharibi na Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania.
Dkt. Kigwangalla amesema kuwa uzinduzi wa hifadhi hiyo mpya ya Taifa ya Burigi wilayani Chato mkoa wa Geita, una nia ya dhati ya kufungua saketi ya Uhifadhi na Utalii Kaskazini-Magharibi badala ya ule wa kaskazini pekee uliozoeleka.
Amebainisha kuwa Sekta ya Utalii ina mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa kutokana na kuingiza fedha nyingi za kigeni ikilinganishwa na sekta zingine, na kwa sasa sekta hiyo inachangia asilimia 17.6 kwenye pato la taifa.