Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Iringa kuanzia tar 29 mwezi huu hadi tar 4 mwezi ujao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa wanatarajia kumpokea rais Dkt. Magufuli kesho tar 29 mwezi huu.
Amesema kuwa mara baada ya kupokelewa Rais Dkt. Magufuli atazindua barabara ya kijiji cha Migori kwenda Fufu kupitia Iringa mjini.
“Siku ya Mei Mosi Rais Dkt. Magufuli atakuwa mgeni rasmi, ambapo kitaifa yatafanyika mkoani hapa ambapo kutakuwepo na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Spika wa bunge na viongozi wengine,”amesema Masenza
Mkuu huyo wa mkoa wa Iringa amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi ambapo zimepangwa kufanyika mkoani humo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Rais Magufuli akiwa ziarani mkoani humo atazindua miradi mbalimbali ya kimaendeleo vikiwemo viwanda.